Jumatano 17 Juni 2026 - 16:15
Amani ya Taifa ni Lulu Inayopaswa Kulindwa na Kuhifadhiwa

Hawza/ Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Mashia nchini Tanzania, Maulana Sheikh Hemed Jalala, amesisitiza umuhimu wa kulinda amani, umoja na mshikamano wa kitaifa, huku akieleza kuwa; amani ni neema kubwa na lulu yenye thamani inayopaswa kutunzwa na kila mwananchi.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Maulana Sheikh Hemed Jalala alitoa wito huo wakati wa hafla ya kuukaribisha mwaka mpya wa Kiislamu wa 1448 Hijria, na ufunguzi wa Majlisi za Muharram, iliyofanyika jana jumnne katika eneo la Kigogo Post, jijini Dar es Salaam, kwa ushiriki wa viongozi wa dini, wanazuoni na waumini mbalimbali.

Akizungumza katika hafla hiyo, Sheikh Jalala aligusia hali ya dunia katika mwaka uliopita, huku akibainisha kuwa; ulimwengu umeshuhudia matukio mengi ya kusikitisha yaliyogubikwa na vita, machafuko na mauaji ya watoto, wanawake na raia wasiokuwa na hatia, hususan katika baadhi ya nchi za Mashariki ya Kati.

Aidha, alielezea matumaini yake ya kuona juhudi za kidiplomasia zikizaa matundahuku akisema kuwa; makubaliano ya amani na maelewano yanapaswa kupewa nafasi ili kuzuia kuendelea kwa umwagaji damu na mateso ya watu wasio na hatia.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake Sheikh Jalala alisisitiza kuwa; amani ya taifa ni miongoni mwa nguzo muhimu za maendeleo na ustawi wa jamii, alikumbusha kuwa Tanzania imeendelea kujijengea sifa ya kuwa kisiwa cha amani barani Afrika, na kwamba ni wajibu wa kila mwananchi kuhakikisha urithi huo unaendelea kuhifadhiwa.

Alisema: “Tanzania imekuwa ikijulikana kwa amani na utulivu wake, tunamuomba Mwenyezi Mungu neema hii iendelee kutawala katika mwaka huu mpya na katika vizazi vijavyo,”.

Sheikh Jalala pia alitoa wito wa kuimarishwa umoja wa kitaifa huku akieleza kuwa; tofauti za dini, makabila au mitazamo havipaswi kuwa sababu ya migawanyiko miongoni mwa wananchi.

Alisisitiza kwamba: Watanzania wote ni sehemu ya taifa moja lenye hatima ya pamoja, hivyo kuna haja ya kuendeleza mshikamano, kuheshimiana na kushirikiana katika kuijenga jamii yenye amani na maendeleo.

Maadhimisho hayo ya kuukaribisha mwaka mpya wa Kiislamu wa 1448 Hijria pamoja na ufunguzi wa Majlisi za Muharram, yaliambatana na dua mbali mbali, nasaha za kidini na wito wa kuendeleza maadili mema, huku washiriki wakihimizwa kuaanza mwaka mpya kwa kuimarisha ucha-Mungu, umoja na kuihudumia jamii.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha